Yaliyojiri
NDANI YA AMANI KUNA UTULIVU; si KILA NDANI YA UTULIVU KUNA AMANI!
Nimesikia serikali ikisisitiza kuwa Tanzania sasa ni tulivu na kila kitu kiko sawa. Tamko hili tamu sana. Lakini kuna haya, yatusaidie kutofautisha utulivu na amani:
1. Sijamsikia kiongozi yeyote wa juu wa serikalini akiongelea utekaji, utesaji, na mauaji. Hata kwa kuigiza, atokee kiongozi alaani vitendo hivi.
2. Nimesikia baadhi ya viongozi wakiongea kwa mafumbo kama ninavyoongea mimi kwamba “lile lililotokea nchini kwetu oktoba 29”. Wanasita hata kulitamka ni jambo gani. Litamkwe ili taifa lipone.
3. Kuna mivutano mingi kati ya taasisi kadhaa na serikali. Mivutano hiyo haijengi. Chanzo twaweza kukijua lakini matokeo yake hatuyajui. Tulidhali Wakatoliki “vijora” ni wa kike, kumbe na wanaume vijora wapo?! Kwaresima ifute vijora wote.
4. Kwa kuwa hakuna anayeongelea utekaji na kutueleza waliotekwa wako wapi, basi angalau fanyeni haya ili tujue kuna amani na si utulivu tu:
i) Acheni watu watekwe lakini wawe HURU kusema kuwa wametekwa. Watekaji wawe na haki ya kuteka; na watekwaji na jamaa zao wawe HURU kupiga kelele.
ii) Watu wafichwe vituo vya polisi vilivyo rasmi na visivyo rasmi bila taarifa, lakini ndugu zao wawe HURU kupiga kelele kuwa ndugu zao wamefichwa.
iii) Watu wabambikiwe kesi lakini wao na ndugu zao wawe HURU kusema wanavyobambikiwa kesi.
iv) Viongozi wawaudhi wananchi na wananchi wawe HURU kununa.
v) Watu waambiwe kwamba kabla hawajaongea na vyombo vya habari wapite serikalini kupatiwa cha kusema, vinginevyo watakutana na ITHIBATI (siyo hisabati).
vi) Watu wawapigie makofi viongozi lakini wawe HURU kusema kuwa wameagizwa washangilie na kupiga makofi.
vii) Wananchi wawe HURU kusema hapakuwa na uchaguzi lakini nchi haiwezi kukaa bila rais kwa hiyo aliyekuwepo anaendelea.
viii) Wananchi wawe HURU kusema uchaguzi ulikuwepo lakini ukavurugwa na kuvuruga matokeo yanayohojiwa. Nchi haiwezi kukaa bila rais. Ndiyo maana yanatafutwa maridhiano kujua kama uchaguzi ulikuwepo au haukuwepo ili tujue tunatokaje.
ix) Wananchi wawe HURU kusema kuwa bunduki inaleta utulivu lakini UHURU unaleta amani. Ndani ya amani kuna utulivu lakini si kila utulivu una amani.
x) Serikali yetu iige hekima ya Kijaluo kwamba, mengine yote tunayo hapa nchini ila kinachokosekana ni UHURU. Kwamba serikali isiporejesha uhuru, na yenyewe haitakuwa HURU. Badala ya kupigiwa makofi, itapigwa makofi.
Mjaluo amehesabu na kugundua kuwa vidhibiti uhuru vimezidi kuwa vingi. Sasa hata wenye magari ya mikopo na ya kuazima yenye namba “A”, mwisho wake ni Kisarawe, Mkuranga, Mlandizi na Bagamoyo. Serikali itawalipia mikopo yao lakini
magari yabaki nje ya jiji!🤣🤣

Maoni